Polisi nchini Kenya wamewakamata zaidi ya waendeshaji 200 wa boda boda katikati mwa jiji la Nairobi huku msako mkali dhidi ya sekta hiyo ukizidi kufuatia unyanyasaji wa kingono wa dereva wa kike kwenye barabara ya Wangari Maathai.
Inspekta Mkuu wa polisi Hillary Mutyambai alitangaza hayo Jumanne. Idadi hiyo iliongezeka kutoka 32. Zaidi ya pikipiki 12 zimezuiliwa.
Hapo awali, polisi walisema ni watu 16 pekee waliotambuliwa na kuhusishwa na shambulio dhidi ya mwanamke huyo.
Video ya dereva huyo wa kike mwenye umri wa 32, akinyanyaswa kimwili na kingono na genge la waendesha bodaboda iliibuka mtandaoni Jumatatu, na kuzua taharuki kwa umma.
Shambulio hilo lilitokea Ijumaa iliyopita saa kumi na moja jioni wakati dereva huyo alipomgonga mwendesha mmoja wa boda boda .
Alisimama mita chache kutoka eneo la tukio, lakini alifukuzwa na kundi la waendesha boda boda , ambao baadhi yao walijaribu kumwibia.
Walimfuata kwa kilomita chache na kulizuia gari lake.
Kisha wakafungua mlango wa gari lake kwa nguvu na mwanamke huyo akapiga mayowe kuomba msaada. Mmoja wa washambuliaji wake, wakati huu wote, alikuwa akirekodi matukio.
Alipoteza pesa na vitu vingine vya thamani kwenye zogo hilo. Aliokolewa na polisi wa trafiki ambao walitahadharishwa na madereva wengine waliokuwa wameshuhudia kisa hicho.
Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang'i alisema "alishtushwa na kuchukizwa" na klipu hiyo ya video.Watu wengi mtandaoni wamelaani kitendo hicho na kuwataka polisi kuwachukulia hatua kali waliohusika
Jaji mkuu wa Kenya Martha Koome akilaani kitendo hicho amesema kuna haja ya kuwalinda wanawake na wasichana dhidi ya visa kama hivyo vya unyanyasaji ili wajihisi salama katika nchi yao .
Koome alisema ni jambo la kusikitisha kwa shambulio hilo kufanyika katika mkesha wa siku ya Kimataifa ya Wanawake.
Amesema mashirika na idara za serikali zinafaa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba visa kama hivyo havitokei .
Leo maandamano yamefanyika jijini Nairobi kulalamikia tukio hilo .Mamia ya watu walijitokeza wakiwa na mabango kutaka hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi ya waendesha boda boda waliomshambulia mwanamke huyon
No comments:
Post a Comment