Mariupol umekuwa mji ulioshambuliwa kwa mabomu na kuharibiwa zaidi katika vita vya Ukraine na Urusi - baada ya kuteswa na mashambulizi ya kudumu ya Urusi. Mji huo ni muhimu kwa kampeni ya kijeshi ya Moscow huko Ukraine. Lakini kwa nini?
Kuna sababu nne kuu kwa nini kuuchukua mji huo wa bandari itakuwa ushindi wa kimkakati kwa Urusi - na pigo kubwa kwa Ukraine.
1. Kupata ukanda wa ardhi kati ya Crimea na Donbas
Kijiografia, jiji la Mariupol linachukua eneo dogo tu kwenye ramani lakini sasa linasimama kwa ukaidi katika njia ya vikosi vya Urusi ambavyo vimetoka kwenye peninsula ya Crimea.
Vinaskukuma kutokea kaskazini-mashariki kujaribu kuungana na wenzao na washirika wanaotaka kujitenga na Ukraine katika eneo la Donbas mashariki mwa Ukraine.
Jenerali Sir Richard Barrons - kamanda wa zamani wa Kamandi ya Vikosi vya Pamoja vya Uingereza - anasema kukamata Mariupol ni muhimu kwa juhudi za vita vya Urusi.
"Warusi wanapohisi kuwa wamemaliza vita hivyo kwa mafanikio, watakuwa wamekamilisha daraja la ardhini kutoka Urusi hadi Crimea na wataona hii kama mafanikio makubwa ya kimkakati."
Iwapo Mariupol itakamatwa, Urusi pia itaishia kuwa na udhibiti kamili wa zaidi ya 80% ya ufuo wa Bahari Nyeusi nchini Ukraine - ikakatisha biashara yake ya baharini na kuitenga zaidi na dunia.
Kwa kuweka utetezi mkali dhidi ya vikosi vinavyosonga mbele kwa muda wa wiki tatu zilizopita, Waukraine wanaotetea wameweza kupambana na idadi kubwa ya wanajeshi wa Urusi. Lakini kushindwa huko kwa Urusi kupata utekaji wa haraka wa jiji hilo, kumewafanya makamanda wa Urusi kuamua kutumia mbinu ya Karne ya 21 kuzingira jiji hilo.
Wameipiga Mariupol kwa silaha, roketi na makombora - kuharibu zaidi ya 90% ya jiji. Pia wamekatiza upatikanaji wa umeme, maji safi, chakula na vifaa vya matibabu - na kusababisha janga la kibinadamu ambalo Moscow sasa inalaumu Ukraine kwa kukataa kusalimu amri kwa makataa ya 05:00 siku ya Jumatatu. Mbunge wa Ukraine ameishutumu Urusi kwa "kujaribu kuiua Mariupol kwa njaa ili kujisalimisha".
Ukraine imeapa kuulinda mji huo hadi mwanajeshi wa mwisho. Inaweza kuja kwa hilo. Wanajeshi wa Urusi wanaingia polepole katikati na, kwa kukosekana kwa aina yoyote ya mpango wa amani unaoweza kutekelezeka, Urusi sasa ina uwezekano wa kuzidisha mashambulizi yake - bila kuibua tofauti yoyote kati ya wanajeshi wanaoutetea mji na raia wanaokabiliwa na hali hiyo ambao ni zaidi ya watu 200,000.
Iwapo, na lini, Urusi itachukua udhibiti kamili wa Mariupol hii itawakomboa karibu wanajeshi wake 6,000 - waliopangwa katika vikundi vya wanajeshi 1,000 - kisha kwenda na kuimarisha pande zingine za Urusi karibu na Ukraine.
Kuna uwezekano mbali mbali wa ni wapi wanaweza kutumwa tena:
• kuelekea kaskazini-mashariki ili kujiunga na vita vya kuzingira na kuharibu vikosi vya kijeshi vya kawaida vya Ukraine vinavyopigana na wanaotaka kujitenga wanaounga mkono Kremlin katika eneo la Donbas.
• kuelekea magharibi kusukuma kuelekea Odesa, ambayo itakuwa sehemu kuu ya mwisho iliyosalia ya Ukraine kuelekea Bahari Nyeusi
• kuelekea kaskazini-magharibi kuelekea jiji la Dnipro
2. Kusakama uchumi wa Ukraine
Mariupol kwa muda mrefu imekuwa bandari muhimu kimkakati kwenye Bahari ya Azov, sehemu ya Bahari Nyeusi.
Pamoja na sehemu zake za kina kirefu, ndiyo bandari kubwa zaidi katika eneo la Bahari ya Azov na nyumbani kampuni kubwa za chuma .Katika nyakati za kawaida, Mariupol ni kitovu kikuu cha mauzo ya nje cha chuma cha Ukraine, makaa ya mawe na mahindi kwenda kwa wateja katika Mashariki ya Kati na kwingineko.
Kwa miaka minane sasa, tangu Moscow kunyakua Crimea kinyume cha sheria mwaka 2014, jiji hilo limekuwa katika hali mbaya kati ya vikosi vya Urusi kwenye peninsula hiyo na waasi wanaounga mkono Kremlin katika jamhuri zilizojitenga za Donetsk na Luhansk.
Kupoteza Mariupol itakuwa pigo kubwa kwa kile kilichosalia katika uchumi wa Ukraine.
3. Fursa ya propaganda
Mariupol ni nyumbani kwa wanamgambo wa Kiukreni wanaoitwa Brigade ya Azov, iliyopewa jina la Bahari ya Azov ambayo inaunganisha Mariupol na Bahari Nyeusi. Kikosi cha Azov Brigade kina watu wenye itikadi kali za mrengo wa kulia wakiwemo Wanazi mamboleo.
Ingawa wanaunda sehemu ndogo tu ya vikosi vya mapigano vya Ukraine, hii imekuwa chombo muhimu cha propaganda kwa Moscow, ikiipa kisingizio cha kuwaambia watu wa Urusi kwamba vijana ambao imewatuma kupigana huko Ukraine wapo ili kuwaondoa wanazi mambo leo .
Iwapo Urusi itafanikiwa kukamata idadi kubwa ya wapiganaji wa Azov Brigade kuna uwezekano wataonyeshwa kwenye vyombo vya habari vinavyodhibitiwa na serikali ya Urusi kama sehemu ya vita vya habari vinavyoendelea vya kuichafua Ukraine na serikali yake.
4. Kukuza motisha
Kutekwa kwa Mariupol na Urusi, ikiwa itatokea, itakuwa muhimu kisaikolojia kwa pande zote mbili katika vita hivi.
Ushindi wa Urusi huko Mariupol utaiwezesha Kremlin kuonyesha raia wake - kupitia vyombo vya habari vinavyodhibitiwa na serikali - kwamba Urusi ilikuwa inafikia malengo yake na na kupiga hatua .
Kwa Rais Putin, ambaye vita hii inaonekana kuwa ya kibinafsi, kuna umuhimu wa kihistoria kwa haya yote. Anauona ufuo wa Bahari Nyeusi wa Ukraine kuwa wa kitu kiitwacho Novorossiya (Urusi Mpya) - ardhi ya Urusi iliyoanzia kwenye himaya ya Karne ya 18.
Putin anataka kufufua dhana hiyo, "kuwaokoa Warusi kutoka kwa udhalimu wa serikali inayoungwa mkono magharibi huko Kyiv" kama anavyoona. Mariupol kwa sasa anasimama katika njia ya yeye kufikia lengo hilo.
Lakini kwa Waukraine, kupoteza Mariupol kutakuwa pigo kubwa - sio tu kijeshi na kiuchumi - lakini pia kwa akili za wanaume na wanawake wanaopigana, wakitetea nchi yao. Mariupol litakuwa jiji kuu la kwanza kuanguka kwa Warusi baada ya Kherson, jiji la kimkakati ambalo halikutetewa sana.
Kuna kipengele kingine cha maadili hapa na ambacho ni cha kuzuia.
Mariupol imeweka upinzani mkali - lakini angalia gharama. Jiji limeharibiwa, kwa kiasi kikubwa liko katika magofu. Itaingia kwenye historia pamoja na Grozny na Aleppo, maeneo ambayo Urusi hatimaye ilishambulia kwa mabomu na kuyarusha chini, na kuyafanya kuwa vifusi. Ujumbe kwa miji mingine ya Kiukreni ni mkali - ukichagua kupinga kama Mariupol ilivyofanya basi unaweza kutarajia hatima sawa.
"Warusi hawakuweza kuingia Mariupol," asema Jenerali Sir Richard Barrons, "hawakuweza kuingia na mizinga yao, kwa hiyo wameipiga na kuwa kifusi. Na hilo ndilo tunalopaswa kutarajia kuona mahali pengine popote ambalo ni muhimu sana kwao."
Mengi zaidi
- YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
- UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
- UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
- KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
- ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
- PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
- SILAHA:Mzozo wa Ukraine:Makombora ya stinger na silaha nyingine kali zinazotumiwa Ukraine
No comments:
Post a Comment