"Jina langu ni Elizabeth Amoaa - ni mwanamke mwenye viungo viwili vya uzazi, nina sehemu mbili za uke yaani via vya uzazi viwili," Mghana mwenye umri wa miaka 38 aliiambia BBC Pidgin, Nunoo mjini Accra.
Sauti yake ikiwa na huzuni wakati anapoelezea jinsi ambavyo amepambana na hali hiyo isiyo ya kawaida ya kiafya.
Hakuwahi kujielewa hadi alipokuwa na umri wa miaka 32 ambapo madaktari waligundua tatizo lake.
Sasa akiwa nchini Uingereza, Bi Amoaa anasema alikaa kwa miaka mingi akiwa na maumivu ya tumbo ambayo mara nyingi yalimfanya ashindwe kufanya kazi kabla ya kugunduliwa kuwa na ugonjwa huo wa ajabu, ambao ni wa asili tu mtu anazaliwa nao.
Aliwahi hata kupata mimba na kujifungua mtoto wa kike kabla hajagundulika mnamo mwaka 2010. Ingawa alikuwa na hedhi alipokuwa mjamzito kwani mfuko wake wa uzazi wa upande pili ulikuwa hauna mimba.
"Ninaweza kuwa mjamzito katika tumbo langu la kulia na bado kupata hedhi kupitia kushoto kwangu. Ndiyo maana nilipokuwa na ujauzito wa binti yangu nilikuwa nikiona damu,” aliiambia BBC.
Baada ya kufanyiwa upasuaji mara nyingi, vipimo na kupata dawa, hatimaye alielewa kilichokuwa kikiendelea katika mwili wake mwaka wa 2015.
Bi Amoaa sasa anataka ulimwengu ujue kuhusu masaibu yake, ili wanawake wengine wasiteseke.
Alikabiliwa na upinzani alipojitokeza hadharani kwa mara ya kwanza kwenye kituo cha redio cha Ghana akizungumzia hali yake, lakini amedhamiria kuelimisha watu.
Ameanzisha shirika la hisani liitwalo Speciallady Awareness na kuandika kitabu, kilichochapishwa Novemba mwaka jana, kuhusu maisha yake.
“Ushauri wangu kwa wanawake wanaopitia hali ya aina yangu ni: usikae kimya; usiteseke kimya kimya; tafuta ufumbuzi wa mapema na matibabu yanayofaa - na kumbuka, wewe ni wa kipekee," aliiambia BBC.
No comments:
Post a Comment