Kwa mujibu wa Shirika la kimataifa la nishati, IEA, bei ya gesi inapanda kwa kasi na kwa mwaka huu inakadiriwa kufikia wastani wa dola $26 kwa kipimo cha MMBTU (Metric Million British Thermal Units). Sababu kubwa ni kupungua kwa usambazaji wa nishati hiyo muhimu.
Nchi za Magharibi pia ziko kwenye harakati za kuiadhibu Urusi kwa kusitisha kununua bidhaa zake ikiwemo Mafuta na gesi kutokana na taifa hilo kuivamia Ukraine.
Kutokana na hilo, mataifa hasa ya magharibi yanayotumia sana gesi asilia yameanza kutafuta suluhisho na njia mbadala ya kupata gesi kwa matumizi ya muda mrefu. Mataifa hayo yameanza kupeleka macho yao kwa wazalishaji wengine wa gesi duniani kama Iran, Qatar na Saudi Arabia kuona wanavyoweza kupata bidhaa hiyo kabla ya kuchukua hatua thabiti ya kuisusa gesi ya Urusi.
Kuna wakati lilitoka wazo la kwamba, kwanza Tanzania ijitosheleze yenyewe kwa gesi yake kabla ya kufikiria kuuza kiwango kikubwa nje ya nchi. Lakini yanayotokea kwenye mzozo wa Ukraine yanaweza kubadilisha mitazamo ya mambo mengi.
Ulaya na gesi ni sawa na 'chanda na pete'
Ulaya wana uhitaji mkubwa wa gesi na mafuta pengine kuliko mabara mengine duniani. Kati ya mapipa milioni tano ya mafuta ambayo husafirishwa nje kila siku duniani, zaidi ya nusu ya hayo huenda Ulaya.
Kwa mujibu wa shirika la kimataifa la nishati, IEA, matumizi ya gesi Ulaya kwa mwaka 2021 yaliongezeka kwa asilimia 5.5% mpaka kufikia mita za ujazo bilioni 552.
Takwimu za CEDIGAZ, zinaonesha Ulaya kwa sasa inapokea takriban asilimia 70 ya mahitaji ya gesi yake kutoka nchi tatu za Urusi, Qatar na Marekani huku ikielezwa makadirio ya asilimia 40 ya mahitaji ya gesi ya bara hilo ni kutoka Urusi na asilimia 30 ya mahitaji yake ya mafuta yanabebwa na taifa hilo linaloongozwa na Rais Vladmir Putin.
Licha ya usambazaji wa gesi ya Urusi kwenda Ulaya kupungua kwa mwaka 2021, lakini kwa kawaida Ulaya inapokea gesi kupitia vituo vyake vikuu vitatu Kondratki cha Poland, Greifswald Ujerumani na Velke Kapusany nchini Slovakia, ambavyo vyote vinapitisha gesi takribani futi za ujazo bilioni 14.3 kwa mwaka.
"Nadhani ikiwa tuko katika ulimwengu ambao mafuta na gesi ya Urusi kuacha kwenda Ulaya basi tutahitaji kuwa na mgao," anasema McWilliams, mchambuzi wa utafiti wa sera ya nishati.
Anachokieleza McWilliams kinaakisi utegemezi wa gesi wa bara hilo kwenye matumizi mengi ya msingi yanayogusa maisha ya watu ya kawaida. Gesi nyingi inayoingizwa hutumika kuzalisha nguvu za umeme gesi, kupikia na magari.
Je Tanzania itaweza kuchangamkia fursa hii?
Hili ni swali ambalo sasa ni mjadala ukihusisha mataifa mengine ya Afrika yanayozalisha gesi kwa wingi kama Nigeria, Algeria, Egypt, Libya na Angola. Je yanaweza kuiona fursa hii na kuichangamkia?
Tanzania ni miongoni mwa nchi 10 zenye akiba kubwa ya gesi barani Afrika ikitajwa kushika nafasi ya 6 kwa akiba yake ya gesi inayokadiriwa kufikia futi za ujazo trilioni 57 sawa na mita za ujazo bilioni 1.6 za hifadhi ya gesi.
Ingawa mahitaji ya gesi Ulaya ni makubwa na hifadhi ya gesi ya taifa hilo la Afrika mashariki ni ndogo ukilinganisha na nchi kama Urusi yenye akiba ya gesi asilia inayofikia mita za ujazo zaidi ya bilioni 700, inaweza kuchangia kapu hilo.
Hivi karibuni rais wa Tanzania, anayesifika kwa kuziona fursa, alinukuliwa akigusia namna mataifa yote ulimwenguni yanavyohaha kutafuta fursa za masoko kwa ajili ya bidhaa zao.
'Iwe Afrika au Ulaya au Marekani, wote tunatafuta masoko', alisema Samia na kuongeza ', kwa bahati mbaya tunafanya kazi na kampuni kutoka Ulaya'.
Ingawa msemo wa waswahili wa 'vita vya panzi, furaha ya kunguru' unaweza usisadifu mazingira ya vita vya Ukraine na Urusi, huenda hii ikawa kete muhimu kwa Tanzania kuanza kufikiria kuiuzia gesi Ulaya.
'Tanzania inaweza kuichangamkia fursa hii ya kuuza gesi yake kwa wingi Ulaya, lakini si rahisi sana kama tunavyodhani, nina wasi wasi kwa sababu biashara ya gesi ni 'umiza kichwa', anasema Prof. Namwata Balthazar mchambuzi na mtafiti wa maendeleo ya jamii. Kwa nini mtafiti huyu anawasiwasi?
Je ina uwezo na utayari na uwezo wa kuibeba fursa hii?
Kuwa tayari ni jambo moja lakini kuweza kutekeleza ni jambo linguine. Pamoja na yote yatakayosemwa, yapo mambo ambayo yataikwaza Tanzania mapema zaidi kabla ya kufikiria kusafirisha kwa wingi gesi yake.
Mosi, ni miundo mbinu ya usafirishaji gesi kwenda Ulaya hiki ni kikwazo kikubwa kwa Tanzania na nchi nyingi hasa za kusini mwa jangwa la sahara zenye hifadhi ya gesi.
"Ili kusafirisha gesi kwa wingi, kwa haraka, kwa usalama na kwa uhakika, unahitaji miundombinu thabiti ya gesi (gas infrastructure) mfano bomba la kuisafirisha gesi. Miundombinu hii ni ghali na inachukua muda mrefu kukamilika' anasema Prof. Balthazar.
Mradi wa bomba la gesi la Nord Stream 2 kutoka Urusi kwenda Ulaya lenye urefu wa kilomita 1,225 (maili 760) kupitia Bahari ya Baltic lilichukua miaka mitano kujengwa na kugharimu $11bn (£8bn).
Wachambuzi wengi wanaona si rahisi kuwa na mbadala wa gesi katika nchi za Ulaya kwa sasa "ni vigumu kuchukua mbadala wa gesi kwa sababu tuna mabomba haya makubwa ambayo yanapeleka gesi ya Urusi kwenda Ulaya," anasema Ben McWilliams,
Pili, Ushindani na wasambazaji wengine, ni jambo lingine kubwa ambalo litaitatiza Tanzania. Yapo mataifa kama Qatar, Iran, Denmark, Saudi Arabia, Australia na China ambayo yana nguvu kiuchumi, kiteknolojia na miundombinu ya kusaidia shughuli za gesi.
Nigeria imeanza ujenzi wa bomba la gesi lenye urefu wa kilomita 614 unaogharimu dola $2.5bn kutoka Ajaokuta-Kaduna mpaka Kano na bomba la gesi la Medgaz huko Algeria ni mfano wa faida ya kibiashara nchi hizo zilizo nayo kwa mazingira ya sasa ya mzozo wa Ukraine kuliko Tanzania.
'Ili kuondoa changamoto hizi, lazima serikali ya Tanzania, ishirikiane na wawekezaji binafsi, na kuunganisha nguvu na mataifa mengine yenye gesi katika ukanda huu kama Angola, Msumbiji, Rwanda na hata Kenya, pamoja na mataifa ya kaskazini (Libya, Misri na Algeria) au magharibi (Nigeria) vinginevyo kuna ugumu kiasi', alisema Prof. Namwata Balthazar
Je taifa hili litaamua kula vilivyoiva kama mmiliki wa kuni ama kula vitamu kwa matokeo ya fursa hii?
No comments:
Post a Comment