Mjadala kuhusu Eneo la uhifadhi la Ngorongoro umekuwa ukiibuka mara kadhaa nchini Tanzania.
Hivi karibuni mamlaka za juu nchini humo zilitangaza hatua kadhaa ikiwemo kuwaondoa watu wa jamii ya wamasai wanaoishi eneo hilo kwa hiari na kuhamia maeneo jirani ambayo yametengwa maalum kwa ajili yao.
Nini Kinaendelea Ngorongoro?
Mgogoro mkubwa kuhusu eneo hili ni kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu na athari zake kimazingira na wanyamapori.
Jamii ya Wamasai wamegawanyika katika makundi mawili, wapo ambao wamekubali kuwa idadi yao ina athari kwa uhifadhi katika eneo hilo. Lakini baadhi yao hawakubali wala hawaoni tatizo la wao kuishi na kuongezeka katika eneo hilo.
Eneo la hifadhi la Ngorongoro ni eneo la urithi wa dunia, eneo hili hukaliwa na Wanyama pori, binadamu na mifugo, na Maisha yao yamekua hivi kwa zaidi ya miongo sita sasa.
Kwa mujibu wa machapisho mbalimbali kutoka shirika la Umoja wa mataifa linaloshughulikia elimu, sayansi na utamaduni UNESCO eneo hili linapaswa kukaliwa na watu wasiozidi 25,000 na malisho ya mifugo na wanyamapori isizidi 254,000.
Lakini takwimu za sasa kutosha mamlaka ya hifadhi ya eneo la Ngorongoro NCAA, wakazi jamii ya wamasai wamefikia 100,000. Ikiwa ni ongezeko kubwa kulingana na mahitaji ya binadamu, mifugo na wanyamapori.
Katika kuhakikisha idadi hiyo ya watu inapungua ili kuondokana na athari za kimazingira, serikali ya Tanzania kupitia Waziri mkuu Kassim Majawaliwa, aliwataka jamii ya wamasai wanaotaka kuondoka kwa hiari kujiandikisha.
Lakini hatua hii ilizua mjadala miongoni mwa jamii ya wamasai wanaoishi katika eneo la hifadhi la Ngorongoro pamoja na wanaharakati kwenye mitandao ya kijamii.
Baadhi wanadai kuwa hatua hii si sahihi na serikali inapaswa kuongea na wananchi wote.
''Ukituhamisha hapa utupeleke wapi?, serikali inapaswa kuongea na wananchi wote, sio viongozi wa kimila pekee, ije izungumze na sisi meza moja, lakini kuondoka hapana'' anasema Joseph mkazi wa Ngorongoro.
Kwa upande mwingine tayari baadhi ya familia zimekubali kujiandikisha na kuondoka eneo hilo.
''Mimi nimekubali kuondoka kwa hiari kwasababu hapa fursa za kiuchumi ni chache, haturuhusiwi kulima na shughuli nyingine za kiuchumi sasa ni bora nikipata eneo nje ya kifadhi'' anasema Samuel Hoho mkazi wa Ngorongoro.
Mgogoro umefika vipi hapa?
Idadi ya wakazi na mifugo yao imekuwa ikiongezeka kila mwaka, Lakini wataalamu wa uhifadhi wanasema mamlaka pamoja na serikali ya Tanzania zimekua na ukakasi wa kuchukua hatua zozote za kuepusha hali kufikia hapa.
Wataalamu wanaongeza kuwa machapisho, tafiti na ripoti mbalimbali kutoka kwa wataalamu pamoja na UNESCO vimekua vikitoa angalizo la idadi ya watu, kuongezeka kwa shughuli za kitalii na suala la mimea vamizi kuwa ni tishio kwa ustawi wa eneo hili ambalo ni urithi wa dunia.
'Kufikia hapa ni kupuuzia kwa tafiti , changamoto kubwa ni utekelezaji wa mapendekezo ya tafiti, tafiti zimekua zikisema kuna tatizo linakuja, lakini hatuheshimu tafiti, wanasayansi tumekua tukisema hii na kuonesha ripoti zetu lakini hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa' Anasema Dkt. Henry Njovu mtaalamu wa ikolojia na uhifadhi.
Anaongeza pia usimamizi wa maeneo kama haya hautakiwi siasa bali kufuata sayansi na utaalamu.
'Wasimamizi wa maeneo kama haya, ipo haja ya wao kufanya kazi zao kisayansi, kwasababu Ikolojia, usimamizi wa wanyamapori ile ni sayansi kwa hiyo kama tukiheshimu sayansi baadhi ya matatizo tunaweza kuepuka na yasitufikishe hapa'' anasema Dkt. Njovu.
Kwanini eneo hili ni muhimu?
Ngorongoro ina umuhimu mkubwa kutokana na kuwa eneo lenye viumbe hai walio hatarini kupotea, lakini pia ni miongoni mwa mahali penye eneo kubwa la kreta duniani. Na mabaki ya zamadamu katika eneo la Olduvai Gorge.
Na kubwa zaidi mwaka 1979 Ngorongoro iliwekwa kwenye orodha ya maeneo ya urithi wa dunia. Lakini pia ni miongoni mwa maeneo ya kustaajabisha duniani kwa vivutio vyake, kuanzia kuhama kwa makundi ya nyumbu na binadamu kuweza kuishi na Wanyama.
Eneo hili limekuwa likisimamiwa na serikali ya Tanzania kupitia mamlaka ya hifadhi NCAA na shirika la UNESCO ambalo mara kadhaa wamekua wakitoa tathmini ya mwenendo wa eneo hilo.
Historia ya Ngorongoro
Kipindi cha ukoloni, eneo hili lilikuwa la shughuli za uwindaji kwa wakoloni. Mwaka 1928 uwindaji huo ukapigwa marafuku eneo la kreta
Ngorongoro ilikuwa sehemu ya Serengeti hadi mwaka 1959, ambapo palitenganishwa na kupewa hadhi tofauti. Ilianzishwa kwa matumizi ya kuishi binadamu, mifugo na Wanyamapori. Wamasai ambao walikuwa wakiishi eneo la Serengeti walihamishiwa katika eneo la hifadhi la Ngorongoro na kuanzisha makazi yao ya kiasili pamoja na kufuga huku wakichangamana na wanyamapori.
Kwa mujibu wa mamlaka ya uhifadhi wa Ngorongoro wakati wa kuanzishwa kwa hifadhi hii kulikuaw na watu 9,000 na mifugo yao 50,000.
No comments:
Post a Comment