WARIDI WA BBC: Ninajiona mrembo licha ya kukosa uwezo wa kutembea kwa miaka 22 - KABATA

This is the special room for news where you need to settle with!


Breaking

Wednesday 9 March 2022

WARIDI WA BBC: Ninajiona mrembo licha ya kukosa uwezo wa kutembea kwa miaka 22

 

Salome Nyakio

CHANZO CHA PICHA,SALOME NYAKIO

Maelezo ya picha,

Salome Nyakio amekosa uwezo wa kutembea kwa miaka 22

Tangu Salome Nyakio alipokuwa na miaka 14 maisha yake yalibadilika kabisa. Sasa hivi akiwa na umri wa miaka 35, hajasahau siku aliyoteleza akiwa amebeba mtungi wa maji na kuumiza uti wa mgongo. Ajali hiyo ilimuacha akiwa amepooza kutoka sehemu ya kifua chake hadi miguuni.

Mwanadada huyo hajatembea kwa miaka 22 ya maisha yake na anasema panda shuka nyingi maishani alizokumbana nazo ndizo zinazompa msukumo wa kuzungumzia haya ili watu waelewe ulimwengu wa kuishi bila uwezo wa kutembea uko vipi.

"Shida kubwa kwangu sio kuwa siwezi kutembea la hasha!", hebu tafakari umepooza kutoka kifuani hadi miguuni, huna hisia yoyote, kumbuka hakuna mawasiliano kati ya ubongo na sehemu zilizopooza. Sasa wewe tafakari kinachoendelea mtu mzima kama mimi anapokosa hisia," Salome anasema.

Na hilo ndilo ambalo limekuwa likimpa msukumo mwanadada huyo kuzungumzia mahangaiko ya wanawake hasa wanooishi na changamoto tofauti tofauti katika miili yao.

Je anamudu vipi bila uwezo wa kutembea?

Salome anaamini kuwa kuna idadi kubwa ya watu haswa ambao hawana uwezo wa kutembea na wanapitia wakati mgumu kutekeleza majukumu ya kawaida ya mwili iwe ni katika haja kubwa au ndogo.

Jambo ambalo linaweza kuonekana kuwa la kawaida kwa binadamu wenye uwezo wa kutembea lakini kwake ni kitu ambacho kimemhangaisha mno.

Mwanadada huyo anasema kwa kuwa hana hisia kuanzia kifuani hadi miguuni, kinachojiri ni kwamba haja zake zote zisipositiriwa kwa vifaa maalum, matokeo yake ni kwamba mwili utatekeleza wajibu wake pasipo yeye kufahamu.

Tangu Salome alipopata ajali hii miaka yote hiyo, amekuwa na changamoto ya kupanga mambo mengi katika maisha yake, lakini pia kupanga kitakachofanyika mwili wake utakapoitisha kwenda haja kubwa au ndogo.

"Ndio ni jambo ambalo sitaona aibu kulisema hadharani, unaona mama mzima kama mimi, inanibidi nitumie taulo za haja kubwa au ndogo za watu wakubwa almaarufu 'diapers' kwa kimombo, hizi taulo ni za bei ghali mno na vilevile zinapojaa unajipata katika shida kubwa kwani harufu nayo itakuwa imeanza. Wakati mwingine utapata kwamba tayari imevuja kwenye nguo. Sio jambo rahisi," Salome anasema.

Miaka ya nyuma wakati mwanadadada huyo alipokuwa anasoma chuo kikuu anataja siku hizo kama zilizojawa na kiza kikuu kwake.

Anakumbuka siku alizokuwa anafunga taulo ya haja na ilipojaa akiwa darasani ikawa ni mtihani kwake.

Salome Nyakio

CHANZO CHA PICHA,SALOME NYAKIO

Salome anatupatia taswira ya siku zilizopita akiwa mwanafunzi chuoni kwamba, wakati wote yeye alikuwa akitumia kiti cha magurudumu, kwa hio hali ya kwamba yuko kwenye kiti hicho na taulo aliyoivaa ikawa imejaa, na maeneo ya kujisaidia yalikuwa hayako karibu na madarasa, kulimpa msongo wa ni vipi atafika maeneo ya kujisaidia kubadilisha na bado aendelee na masomo darasani.

Salome anasema hawezi kuhesabu ni siku ngapi wanafunzi wenzake darasani hawakuwa wanamsogelea kwasababu anatoa harufu mbaya za kuvuja kwa haja ndogo ila hana la kufanya.

Vile vile anatoa taswira ya mahangaiko ya kuvaa taulo na jinsi inavyo mchoma mtu hasa iwapo ataivaa kwa muda mrefu bila kubadilisha kwa wakati ufaao.

"Kusema ukweli jambo hili siwezi kumtakia hata adui wangu. kutokuwa na uwezo wa kutumia miguu kunaniweka kwenye gharama kubwa na vile vile mahangaiko ila najituliza kwa kusema huenda sielewi ni kwanini mimi ndio nilipata ajali na kupoteza nguvu ya miguu yangu. Lakini je kuna mtu ambaye hujitakia mabaya duniani? hapana, ndio maana nimekubali hali yangu na kila siku ninaishi kwa kupigania ulimwengu wetu ueleweke." anasema Salome.

Japo mwanadada huyo anasema kwamba kwa miaka ya hivi karibuni hatumii tena taulo za kujisaidia haja zake za kimwiIi, badala yake anatumia teknolojia nyengine ambazo zinagharimu mamia ya fedha na vile vile zinahitaji ustadi kutumia kwani ni vifaa ambavyo vinauwezo wa kumletea mtu madhara mengine ya kiafya.

Ari ya kujaaliwa mtoto

Licha ya changamoto anazoishi nazo, Salome anasema kwamba maumbile ya kawaida ya mwanamke kutamani kuwa mlezi, kutamani mtoto na ndoa sio vitu ambavyo vimemuepuka, hivyo basi aliheshimu hisia zake na kujaaliwa mtoto.

Anakubali kwamba wengi ni wale waliokuwa wanamshangaa ni vipi mwanadada kama yeye mwenye changamoto za kutembea atajiweka kwenye majukumu mengine ya kuitwa mama?

Salome anasema kwamba sio wengi walioelewa chaguo lake la kuingia kwenye mahusiano ya kimapenzi yaliopelekea yeye kushika mimba.

"Shida ni kuwa kwa watu kama sisi wanaoishi na changamoto za maumbile, mara nyingi tutapata wanaume ambao hawatupendi kutoka moyoni ila wanaona ni kana kwamba wanatusaidia," Salome anasema.

Na alifanikiwa kushika mimba wakati alitamani lakini kulikuwa na changamoto nyingi zilizoendana na yeye kubeba ujauzito huo, hasa kwa kuwa mara nyingi yuko kwenye kiti kinachomuwezesha kusonga kutoka sehemu moja hadi nyingine.

Ilimlazimu mtoto wake kuzaliwa kwa njia ya upasuaji. Anasema kwamba ujauzito kwake ulikuwa mzito ila kumlea mtoto wake ilikuwa rahisi.

Alikubali changamoto zilizoandamana nazo kwa mfano kumnyonyesha mtoto na hata kumbadilisha nepi baada ya haja zake huku akiwa kwenye kiti cha magurudumu.

Mwanadada huyo anatudhihirishia kwamba alikutana na mwanamume aliyempenda licha ya changamoto zake.

Anasema kwamba walikutana, wakapendana na kuwa wapenzi lakini mambo kati yao hayakwenda vizuri.

Baada ya muda waliamua kutengana na hapo ndipo Salome alipoamua kuanza maisha yake kama mzazi mlezi wa kipekee kwa mwanae wa kiume ambaye sasa hivi ana miaka minne.

Salome anasema wakati watu kama yeye wawe ni wa jinsia ya kike au kiume wanatafuta kupendwa, mara nyingi wanakumbana na changamoto ya ulemavu wao kupewa kipau mbele badala ya utu.

''kwa mfano wengi ni wale wanakutana na mimi, kitu cha kwanza watu hugundua ni kiti cha magurudumu na kwa hiyo kila kitu kitazungukia ulemavu wangu na wala sio mimi ambaye natumia kiti hicho. Kwa hiyo kunakuwa na changamoto ya kuwa na mwenza aliyekubali maumbile hayo, " anasema Salome.

Na hilo ndio lililochangia kuvunjika kwa uhusiano wake baada ya kuhisi kuwa hakupendwa kwa dhati.

Historia ya ajali

Salome Nyakio

CHANZO CHA PICHA,SALOME NYAKIO

Wazazi wake Salome walifariki akiwa na umri wa miaka minane. Yeye pamoja na ndugu zake wawili wamepata malezi ya utotoni kutoka kwa bibi yao. Lakini Salome alipata ajali wakati anaishi na mjomba wake akiwa na miaka, 14.

Ulikuwa ni mwaka ambao alifanya mtihani wake mkuu kukamilisha masomo ya shule ya msingi. Kipindi hicho alikuwa anasubiri kuingia shule ya sekondari asijue kwamba ajali aliyoipata ingehairisha ndoto hio kwa miaka mitano mbele.

Mwanamke huyo anasema kwamba aliteleza akiwa amebeba mtungi wa maji mngongoni. Eneo aliloteleza lilikuwa ni timboni na anakumbuka akiangukia jiwe lililomuumiza vibaya kwenye uti wake wa mgongo.

Mahangaiko yake yalianza hapo na kwa miezi 23 baada ya siku ya ajali alikuwa bado yupo kwenye hospitali aliyopelekwa kupata matibabu huko nchini Kenya.

Ilichukua muda kwake kujikubali kwamba hatatembea tena licha ya matibabu aliyoyapata.

Salome anasema kwamba alijiuliza maswali mengi kwa mfano mbona yeye tu ndio alipata ajali hio? ila pia alianza kujiuliza iwapo sio mimi ni nani mwengine? na kujipa nguvu ya kuanza maisha mapya ambayo ni kutumia kiti cha magurudumu daima.

Ilikusaidia jamii katika uelewa wa hali ya watu wanaoishi na mapungufu katika maumbile yao, Salome alianza kutumia mitandao ya kijami kama njia rahisi ya kuelemisha umma hasa kupitia simulizi ya maisha yake ya kila siku.

Salome pia ana uhusiano wa karibu na jamii inayomzunguka kwani huwa ana hutubia maeneo tofauti tofauti na hata katika shule mbalimbali nchini Kenya kama njia moja ya kuelimisha wengine.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here